Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa Walenga Kuongeza Matumizi ya aina 13 ya Bidhaa za afya

Umoja wa Mataifa Walenga Kuongeza Matumizi ya aina 13 ya Bidhaa za afya

Wanakamati wa Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu bidhaa za kuokoa maisha ya wanawake na watoto, wamekutana leo kwenye makao makuu New York kurejelea na kukamilisha mapendekezo ambayo yatasaidia kuongeza usambazaji, kupunguza gharama na kuongeza uvutio wa hadi bidhaa 13 tofauti.

Tume hiyo inayosimamiwa na rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, inalenga kusaidia kuondoa vizuizi katika uzalishaji, usambazaji na matumizi mazuri ya aina 13 za bidhaa ambazo mara nyingi zinapuuzwa, ingawa zina uwezo wa kuokoa maisha. Baadhi ya bidhaa hizi ni oxytocin inayowazuia akina mama kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua, dawa zenye chumvi za kuongeza maji kwa watoto wenye kuharisha, na amoxicillin yenye kutibu nimonia au kichomi.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema ni lazima mapendekezo ya tume hiyo ambayo yatachapishwa mnamo mwezi Septemba, ni yaangazie bidhaa zote kwa jumla zenye uwezo wa kuokoa maisha.