Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wote wanastahili haki sawa bila kujali hisia za mapenzi:Pillay

Watu wote wanastahili haki sawa bila kujali hisia za mapenzi:Pillay

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Bi Navi Pillay, amezikashifu sheria zinazowabagua watu wenye kufanya mapenzi ya jinsia moja kote duniani, na kutoa wito zibadilishwe sheria hizi ili kuwepo usawa. Bi Pillay amesema haya hii leo, ambayo ni siku ya kimataifa dhidi ya ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

Kamishna Pillay pia amesema katika taarifa ilotolewa leo kuwa baadhi ya watu husema kuwa anachochea kuwekwe aina mpya au maalum za haki kila anapolizungumzia suala hili, lakini hakuna lolote jipya au maalum kuhusu haki ya kuishi na ya kuwa na usalama, na haki ya kuwa na uhuru wa kutobaguliwa.

Ameongeza kuwa kote duniani watu hukamatwa, hushambuliwa, na wengine kuteswa au hata kuuawa kwa sababu wana uhusiano wa kimapenzi na mtu wa jinsia yao. Afisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imetoa video fupi kwenye YouTube, inayohimiza usawa na haki kwa watu wote bila kuzingatia mienendo yao ya kimapenzi au jinsia.