Kamanda wa LRA anayehusika na Ukiukaji wa Haki dhidi ya Watoto akamatwa

14 Mei 2012

Jeshi la Uganda limemkamata Caesar Acellam Otto, mmoja kati ya viongozi wa juu wa kijeshi wa kundi la Lord’s Resistance Army LRA. Mtu huyo amekamatwa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Acellam pamoja na kiongozi mkuu wa LRa Joseph Kony na makamanda wengine wa kundi hilo wanahusika na uhalifu mkubwa uliotekelezwa dhidi ya watoto katika eneo la Afrika ya Kati.

Mwakilishi wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya watoto kwenye maeneo ya vita vya silaha, Bi Radhika Coomaraswamy, amesema ametiwa moyo na kukamatwa kwa kamanda huyo na anatumaini serikali ya Uganda haitompa msamaha na badala yake kumfikisha mbele ya sheria.

Amesema kuwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria kutatoa ujumbe muhimu kwa uongozi wa LRA kwamba watawajibishwa kwa matendo yao.

Sheria ya msamaha ya Uganda inatoa fursa ya msamaha kwa wafuasi wa LRA ikiwemo ule wa makosa ya uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na ukiukaji wa haki za binadamu.

Acellam amekamatwa pamoja na mkewe, mwanawe na binti wa miaka 12 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambaye wajibu wake haujajulikana. Familia hiyo hivi sasa inashikiliwa na serikali ya Uganda huko Sudan Kusini. Kundi la LRA linaelezewa kuwa na waasi wapatao 200 hadi 500 wanaoendesha uasi Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter