Mtalaamu wa UM kuchunguza haki za binadamu Azerbaijan

Mtalaamu wa UM kuchunguza haki za binadamu Azerbaijan

Mtaalam maalumu wa Umoja wa Mataifa, Anand Grover ataizuru Azerbaijan tokea tarehe 16 hadi 23 Mei mwaka huu, kuchunguza maswala ya kuhakikisha haki za kiafya nchini humo, na hasa zile zinazohusiana na kugharamia afya, kifua kikuu, pamoja na maswala ya afya katika magereza na vituo vya kuwazuilia watu. Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni tishio kubwa nchini Azerbaijan, ambako kuna viwango vya juu vya aina za ugonjwa huo ambazo ni ngumu kutibu.

Ziara ya Bwana Grover nchini Azerbaijan ndiyo ya kwanza ya Mtaalam huru kuwahi kupelekwa huko na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa minajili ya kukagua haki za watu wote kuwa na afya ya hali ya juu. Bwana Grover atazingatia maswala ya ubaguzi na unyanyapaa, ambayo anasema ni muhimu katika kuhakikisha ugonjwa wa Kifua Kikuu hausambazwi zaidi. Atakutana na maafisa wa serikali, wabunge, wawakilishi wa kimataifa, maafisa wa afya pamoja na wawakilishi wa mashirika ya umma.