Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanajeshi wa zamani wa SPLA wafuzu mafunzo chini ya mpango wa IOM

Wanajeshi wa zamani wa SPLA wafuzu mafunzo chini ya mpango wa IOM

Kundi la watu 285 ambao ni wanajeshi wa zamani wa SPLA Sudan ya Kusini, wamefuzu wiki hii baada ya kupata mafunzo ya ufundi katika kozi mbalimbali, zenye lengo la kuwarejesha katika maisha ya kawaida kama uraia katika jimbo la Equatoria Mashariki.

Kozi hizo ambazo zimefadhiliwa na tume ya kurejesha silaha na uwiano, ikishirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP na Afisi ya Uhamiaji ya Umoja huo, zimewawezesha jumla ya wanajeshi 5, 755 wa zamani kote nchini kufuzu katika kipindi cha miezi tano ilopita.

Kama sehemu ya mpango unaogharamiwa na UNDP, IOM inatoa usaidizi kwa wanajeshi wa zamani katika kukuza ujuzi na kutoa vifaa vya kujiwezesha kupata riziki na kuboresha hali yao ya kiuchumi, pamoja na kuwapa kipato cha kutosha kuwawezesha kurejelea maisha ya kawaida. Kuingizwa kwao katika maisha haya pia kunasaidia katika kukuza jamii zao.

Mpango huo uliozinduliwa mwaka 2010, ulilenga watu

12,525. Hivi sasa IOM imewasaidia zaidi nusu ya wanajeshi wote katika majimbo manne kati ya kumi ya Sudan Kusini, yakiwemo Warrap, Bahr el Ghazal Magharibi, Bahr el Ghazal Kaskazini na Equatoria Mashariki. Walofuzu wiki hii walipewa mafunzo ya udereva, ufanyibiashara mdogo, utengenezaji wa vyakula, umakanika na useremala.