Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bi Pillay asema ni sawa Sudan Kusini kuzingatia kulinda haki za binadamu, ingawa juhudi zaidi zastahili kufanywa

Bi Pillay asema ni sawa Sudan Kusini kuzingatia kulinda haki za binadamu, ingawa juhudi zaidi zastahili kufanywa

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Bi Navi Pillay, amesema kuwa ni sharti serikali ya Sudan Kusini kujaribu kwa vyovyote vile kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa nchini humo. Bi Pillay ambaye yumo ziarani nchini Sudan Kusini amesisitiza kuwa haijalishi ni muda gani taifa limekuwepo, na haki za binadamu ni lazima zilindwe, bila kuwa na sababu yoyote ya kuzikiuka au kutozizingatia.

Ameunga mkono juhudi zinazofanywa hivi sasa na serikali ya Sudan Kusini katika kulinda haki za binadamu, lakini akaongeza kuwa mengi bado yanastahili kufanywa. Bi Pillay amesema, anatarajia kuwa ziara yake itaichagiza serikali ya Sudan Kusini kuweka saini mikataba muhimu ya kulinda haki za watoto, watu wenye ulemavu, wafanyakazi wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi. Pia anataraji kuwa itasainiwa kwa haraka mikataba ya kulinda haki dhidi ya dhuluma, kuwanyanyasa wanawake na ubaguzi wa rangi, pamoja na ile ya kulinda haki za msingi za binadamu.