Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunisia lazima ilinde haki za binadamu ikiwemo ya elimu:UM

Tunisia lazima ilinde haki za binadamu ikiwemo ya elimu:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya elimu Kishore Singh leo ameitaka serikali ya Tunisia kuifanya nchi hiyo iendelee kudumisha historia kwa kutoa kipaumbele katika masuala ya haki za binadamu na haki ya elimu katika mabadiliko yanayotokea hivi sasa.

Tunisia iko katika mabadiliko makubwa kihistoria amesema bwana Singh wakati akikamilisha ziara yake ya kwanza ya kupata ukweli nchini humo.

Amesema endapo nchi hiyo ikishindwa kupata katiba mpya na sheria mpya kutokuwa na viwango vinavyostahili kulinda haki za binadamu, hususani haki ya elimu, basi Tunisia itakosa fursa muhimu ya kihistoria.

Amesema wakati ni sasa kwa serikali ya nchi hiyo kulinda mabadiliko na kujihami tayari kwa kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mtaaaamu huyo huru wa haki ameikumbusha serikali wajibu wake wa kuhakikisha na kulinda uhuru wa elimu katika taifa hilo ambalo ghasia zilizochochewa na makundi ya kidini yenye itikadi kali zimetokea hivi karibuni kwenye vyuo vikuu.