Sudan yawataka raia 12,000 wa Sudan Kusini kuondoka

30 Aprili 2012

Serikali ya Sudan imesema zaidi ya raia 12,000 wa Sudan Kusini wanapaswa kuondoka nchini humo katika kipindi cha wiki moja. Kwa mujibu wa gavana wa jimbo la White Nile kuwepo kwa raia hao katika eneo la Sudan kunasababisha tishio la usalama.

Sudan na Sudan Kusini hivi karibuni zimekuwa katika mzozo kuhusu eneo la mpakani lenye utajiri wa mafuta. Gavana huyo ameongeza kuwa serikali ya Sudan Kusini ilikubali kuwahamisha raia wake zaidi ya mwaka mmoja uliopita, na wengi wa raia hao wa Kusini walihamia Kaskazini baada ya mkataba wa mwaka 2002 ili kutafuta ajira.

Maelfu ya raia hao hivi sasa wako njiani kuelekea nyumbani lakini wengine wamekwama karibu na mpaka wa Sudan Kusini. Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wamekuwa wakishirikiana kufanikisha kuwarejesha nyumbani maelfu ya raia hao wa Sudan Kusini.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter