Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu ya Charles Taylor kutolewa Alhamisi

Hukumu ya Charles Taylor kutolewa Alhamisi

Hukumu ya kesi dhidi ya Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor inatarajiwa kutolewa Alhamisi Aprili 26. Majaji katika mahakama maalumu ya Sierra Leone watatoa hukumu ya endapo Rais huyo wa zamani ana hatia ya uhalifu wa vita uliotekelezwa wakati wa vita vya wenye kwa wenyewe nchini Sierra Leona ama la.

Kesi hiyo imeendeshwa kwa miaka mitano sasa baada ya Taylor kushitakiwa na mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa akidaiwa kuchochea vita vya Sierra Leone mwaka 1991 hadi 2002. Anakabiliwa na makosa 11 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo ubakaji, utumwa wa ngono, kuwatishia raia na kuwaingiza watoto jeshini.

Wakati wa kesi mahakama imesikia ushahidi wa watu zaidi wa 90 akiwemo mrimbende Naomi Campbell kuhusu zawadi ya almasi aliyopewa na Taylor.

Watu zaidi ya 50,000 waliuawa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe wengine viungo vyao kukatwa na kusalia na vilema vya maisha. Taylor aliachia madaraka 2003 na kuishi uhamishoni Nigeria hadi alipokamatwa 2006.