Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uongozi wa Syria watakiwa kuongeza juhudi kumaliza machafuko

Uongozi wa Syria watakiwa kuongeza juhudi kumaliza machafuko

Uongozi wa Syria unapaswa kuacha mara moja kutumia silaha nzitonzito na kuondoa wanajeshi wake kutoka maeneo ya raia. Hivyo ndivyo mkuu wa idara ya siasa ya Umoja wa Mataifa Lynn Pascoe alivyoliambia Baraza la Usalama Jumatatu wakati wa kikao kuhusu Mashariki ya Kati.

Serikali ya Syria imekubali kusitisha machafuko kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo sita ya mpango wa amani uliopendekezwa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu Kofi Annan.

Bwana Pascoe amesema jumuiya ya Kimataifa kwa sasa iko katika kile alichokiita wakati muhimu sana nchini Syria. Jumamosi Baraza la Usalama liliidhinisha mpango wa uangalizi Syria UNSMIS kutokana na pendekezo la Katibu Mku la kupeleka wanajeshi 300 wasio na silaha nchini humo.

Tayari kuna timu ya waangalizi saba waliokwisha wasili Syria ambako kumekuwa na maandamano kwa zaidi ya mwaka sasa wakipinga utawala wa Rais Bashar al-Assad.