Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Selena Gomez atoa wito wa hatua za kuokoa maisha kwa niaba ya watoto wa Sahel

Selena Gomez atoa wito wa hatua za kuokoa maisha kwa niaba ya watoto wa Sahel

Muigizaji, muimbaji mashuhuri na mbunifu wa mitindo ambaye ni balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Selena Gomez anatumia umaarufu wake katika kampeni ya UNICEF ya kuokoa maisha katika eneo la Sahel Afrika ya Kati na Magharibi.

Bi Gomes amesema hali inahitaji hatua za dharura Sahel na watoto wa eneo hilo wanahitaji msaada wa haraka. Amewataka watu kujua kwamba kwa pamoja na UNICEF wana uwezo wa kuzuia vifo zaidi kwenye eneo hilo.

Wiki iliyopita alitumia mtandao kupitia anwani yake ya twitter iliyo na wafuasi zaidi ya milioni 11 kuchagiza wito wa kimataifa wa kuchangia fedha zitakazotumika kuzuia vifo vya mamilioni ya watoto kutokana na utapia mlo. Bi Gomez pia amerekodi ujumbe unaowachagiza vijana kuchanga dola 10 kupitia ujumbe wa simu ya mkononi kusaidia kuepuka janga Sahel. Aliteuliwa kuwa balozi mwema wa UNICEF mwaka 2009 na amekuwa akitumia kipaji chake kuelezea matatizo yanayowakabili watoto.