Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maafisa wa UM na Muungano wa Afrika wakutana na waathiriwa wa dhuluma za kundi la LRA

Maafisa wa UM na Muungano wa Afrika wakutana na waathiriwa wa dhuluma za kundi la LRA

Maafisa wa ngazi za juju kutoka Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wamekutana na waathiriwa wa visa vya kundi la Lord’s Resistance Army LRA kwenye eneo la Dungu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambapo waliwahakikishia kuwa watafanya kila jitihada kuhakikisha dhuluma za kundi hilo zimekomeshwa.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa eneo la Afrika ya Kati Abou Moussa amewaambia waathiriwa hao kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa wamerudi makwao na kuendelea na shughuli zao za kawaida. Kundi la LRA lililobuniwa miaka ya themanini limekuwa likiwalenga raia wa Uganda na vikosi vya usalama kwa muda wa miaka 15 kabla ya kuvuka na kuingia nchi majirani likiendesha dhuluma zikiwemo ubakaji, mauaji na utekaji nyara wa watoto na kuwaingiza jeshini.