Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na AU kuimarisha mpango wa kukabiliana na kundi la LRA

UM na AU kuimarisha mpango wa kukabiliana na kundi la LRA

Maafisa wa ngazi za juu kutoka Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wanazuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kuimarisha mpango mpya wa pamoja uliozinduliwa kukabiliana na tishio la kundi la kigaidi la waasi wa Uganda lijulikanalo kama Lord’s Resistancy Army (LRA)

Wakiwa nchini Dr Congo mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Abou Moussa na mwakilishi wa muungano wa Afrika kuhusu suala la LRA Francisco Madeira watakuwa na kikao maalumu mjini Kinshasa na uongozi wa serikali ya Dr Congo, uongozi wa kikanda na washirika wa kimataifa wanaohusika katika vita dhidi ya LRA kundi ambalo muungano wa Afrika unaliita la kigaidi.

Katika siku sita za ziara yao iliyoanza jana maafisa hao wawili watakwenda pia eneo la Dungu Kaskazini Mashariki mwa DR Congo kwenye jimbo la Orientale ambako kikosi cha kikanda cha RTF kilichopewa dhamana na muungano wa Afrika kulisaka kundi la LRA kitakuwa na makao yake.

Zaidi ya watu watu 4200 wametawanywa kutokana na mashambulizi ya LRA kwenye jimbo la Orientale tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Kundi la LRA lilianzishwa miaka ya 1980 nchini Uganda na kwa zaidi ya miaka 15 mashambulizi yake yamekuwa ni dhidi ya raia wa Uganda na vikosi vya usalama ambayo mwaka 2002 vilifurusha kundi hilo na ndipo lilipohamishia shughuli zake kwa nchi majirani wa Uganda kwa kutekeleza vitendo kama kuwaingiza watoto jeshini, ubakaji, mauaji , ukatili na kuwageuza watu kuwa watumwa wa ngono.

Ijumaa wakitoka Dungu wawakilishi hao watakwenda Kusini Mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako kikosi kingine cha RTF kitakuwa na makao yake. Maafisa hao huko watakutana na wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Uganda ambako hivi sasa wako katika operesheni za kukabiliana na LRA kwa msaada wa kikosi cha kijeshi cha Marekani.