Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais mpya wa Malawi ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake

Rais mpya wa Malawi ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake

Mwanaharakati wa kupigania haki za wanawake nchini Malawi Joyce Banda amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais Kusini mwa Afrika baada ya kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha Rais Bingu wa Mutharika.

Mwanamama huyo aliyekuwa makamu wa Rais na mama wa watoto watatu ameapishwa Jumamosi kwa mujibu wa katiba kuliongoza taifa hilo ambalo ni miongoni mwa nchi masikini barani Afrika.

Joyce mwenye umri wa miaka 61anafahamika kama mlezi na mama kwenye jamii ni mtaalamu wa masuala ya uzazi tofauti na Rais aliyemtangulia aliyejulikana zaidi kama mkuu wa masuala ya kiuchumi.

Bi Banda ambaye ameshawahi kujishindia tuzo kutokana na kazi zake za kupigania haki za wanawake mwaka jana alitajwa na jarida la Forbes kama mwanamke wa tatu shupavu na mwenye ushawishi wa kisiasa Afrika baada ya Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf na waziri wa fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala.

Hadi sasa Bi Banda ambaye ni mtoto wa afisa wa polisi amekuwa akitumia muda wake mwingi kufanya kampeni kwa ajili ya wanawake wa vijijini. Na amekuwa akieleza bayana lengo lake ni kuwakomboa wanawake wa nchi masikini Afrika kutoka kwenye mzunguko wa umasikini na ukatili uliowaghubika kwa karne na karne.