Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataja vipaumbele vya kuwasaidia watu wenye matatizo ya mtindio wa ubongo

Ban ataja vipaumbele vya kuwasaidia watu wenye matatizo ya mtindio wa ubongo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameahidi kuendelea kutoa msukumo wa pekee kuzisaidia jamii za watu zinazokabiliwa na tatizo la ugonjwa wa akili ambao wakati mwingine hawapewi zingatio la kutosha.

Amesema Umoja wa Mataifa umedhamiria kwa dhati kuendelea kuhamasisha jamii ili kutambua changamoto zinazowakabili watu wa namna hiyo ambao mara zote wanaachwa kando.

Katika hatua zake za kwanza, tayari Umoja wa Mataifa umeanza kusambaza stempu kadhaa ambazo zimebeba ujumbe maalumu wa watu wenye matatizo ya akili hasa matatizo ya utotoni.

Bahasha hizo zimeanza kuuzwa katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko New York, Geneva na Vienna.

Stempu hizo zimechagizwa na kazi maalumu za ubunifu ambazo zinadaiwa kufanywa na watu wenye matatizo hayo.

Ban amesema kuanza kusambazwa kwa stempu hizo kunatuma ujumbe masusi kwa makundi ya watu duniani kote namna makundi hayo ya watu walivyo na uwezo mkubwa.