Baraza la Usalama lavitolea mwito vyama vya kisiasa nchini Guinea-Bissau

2 Aprili 2012

Baraza la Usalama limevitolea mwito vyama vya kisiasa nchini Guinea-Bissau kuingia kwenye meza ya majadiliano ili kufanikisha duru ya pili ya uchaguzi mkuu ulio usoni.

Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika baadaye mwezi huu wanne, ni mwendelezo wa harakati za kisiasa zilizoanza mwezi January mwaka huu. Baraza hilo la usalama linataka uchaguzi huo unaokuja unafanyika katika mazingira ya haki na amani na pande zote kuweka mazingira ya kuaminiana.

Limewataka viongozi wa kisiasa pamoja na wafuasi wake, kujiepusha na matukio ambayo yanaweza kuvuruga hali ya utengamao na amani na hivyo kurudisha nyuma demokrasia ya nchi hiyo.

Nchi hiyo iliyoko Afrika magharibi inapitia kipindi cha mpito kufuatia kufariki dunia kwa rais Malam Bacai Sanhá aliyeaga dunia January mwaka huu na hivyo kulazimika kufanyika kwa uchaguzi wa mapema.

Duru la pili la uchaguzi huo limepangwa kufanyika tarehe 22 mwezi huu wane, ikiwakutanisha baina ya waziri mkuu wa zamani Carlos Gomes Junior na rais wa zamani Kumba Yala.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud