ICTR yaamuru mshtakiwa wa mauaji ya Rwanda arejeshwe Kigali

27 Machi 2012

Mahakama ya Umoja wa Mataifa ambayo inaendesha kesi dhidi ya watuhumiwa muhimu waliohusika kwenye mauwaji ya mwaka 1994 nchini Rwanda, imetaka mashauri juu ya watuhumiwa kadhaa waliosalia yahamishiwe katika mahakama kuu ya Rwanda.

Mahakama hiyo kwa ajili ya uhalifu wa kivita wa Rwanda ICTR, imeamuru keshi dhidi ya mtuhumiwa Charles Sikubwabo irejeshwe nchini Rwanda na kusikilizwa na mahakama kuu ya huko.

Bwana Sikubwabo, ambaye ni meya wa zamani wa jimbo la Gishyita lililoko kusini mwa Kibuye anashtakiwa kwa kupalilia mauwaji hayo ya halaiki na uharibifu dhidi ya binadamu.

Mapema mwezi Novemba mwaka jana, waendesha mashtaka katika kesi hiyo waliomba mahakama hiyo ya ICTR iruhusu mtuhumiwa huyo arejeshwe katika mahakama ya Rwanda.

Ikitangaza uamuzi wa kurejeshwa nchini Rwanda, ICTC imetaka mshtakiwa huyo akabidhiwe kwa waendesha mashtaka kwa Rwanda, katika kipindi kisichozidi siku 30 tangu kutolewa kwa uamuzi huo.

Mahakama hiyo ya ICTR iko mjini Arusha nchini Tanzania.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter