Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA kupata msaada kutoka Marekani

UNRWA kupata msaada kutoka Marekani

Mshauri maaluum wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton kuhusu masuala ya kimataifa ya vijana ametangaza kwenye mkutano wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA ongezeko la msaada wa dola milioni 10 kwa mfuko wa shirika hilo.

Ongezeko hilo litafanya mchango wa serikali ya Marekani kwa UNRWA mwaka 2012 kufikia dola milioni 65.

Marekani inasema msaada huo ni muhimu kwa shughuli za UNRWA hasa zinazohusisha vijana ikiwa ni pamoja na mahitaji ya elimu kwa watoto zaidi ya 480,000 ambao wanahudhuria shule za UNRWA.

Mshauri huyo Ronan Farrow ameitaka UNRWA kutoa fursa kwa vijana wakimbizi wa Kipalestina kushiriki majadiliano ya mipango na miradi ya UNRWA.

Naye kamishina mkuu wa UNRWA Filippo Grandi ametoa shukrani za dhati kwa Marekani kwa mchango huo na kusema umekuja katika wakati muafaka kwa wakimbizi wa Kipalestina.