Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waonya kuhusu uhusiano baina ya ubaguzi wa rangi na migogoro

UM waonya kuhusu uhusiano baina ya ubaguzi wa rangi na migogoro

Maafisa wa ngazi ya juu wameonya kuhusu hatari ya uhsiano baina ya ubaguzi wa rangi na vita, wakiitaka jumuiya ya kimataifa kushughulikia dalili za hali hiyo kabla haijawa janga kubwa la mgogoro.

Katika ujumbe wake kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ubaguzi wa rangi na ubaguzi mwingine vimekuwa vikitumiwa kama silaha za kuleta hofu na chuki, na katika hali zingine viongozi wasiofaa huchochea ubaguzi unaosababisha mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ubaguzi wa rangi na vita, ikisistiza kwamba ubaguzi wa rangi unaweka hatarini amani, usalama, haki na maendeleo ya jamii.

Naye kamishina mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay amesema uhusiano uliopo baina ya ubaguzi wa rangi na migogoro ni mizizi iliyojikita kwa muda mrefu ambayo inapaswa kung’olewa.

(SAUTI YA NAVI PILLAY)

Tarehe 21 Machi ya kila mwaka Umoja wa mataifa unaadhimisha siku hii ambapo inakmbuka mwaka 1960 pale makumi ya watu waliokuwa wakiandamana kwa amani walipopigwa risasi na kuuawa na polisi wa Afrika ya Kusini kwenye kitongoji cha Sharpeville wakiandamana kupinga ubaguzi wa rangi.