Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watu wanaokimbia mapigano nchini Mali yaongezeka: OCHA

Idadi ya watu wanaokimbia mapigano nchini Mali yaongezeka: OCHA

 

Shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA linasema kuwa idadi ya watu waliolazimika kuhama makwao nchini Mali inazidi kuongezeka wakati hadi sasa watu 195,000 wakiwa wamehama ambao 100,000 kati yao wakiwa ni wakimbizi wa ndani na wengine 95,000 wakikimbilia Mauritania, Burkina Faso na Niger.

OCHA inakadiria kuwa huenda watu 200,000 wakalazimika kuhama makwao ikiwa ghasia zilizopo zitaendelea.

Nao mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 2.6 kwa mashirika yakiwemo shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, shirika la mpango wa chakula duniani WFP na lile la kilimo na mazao la Umoja wa Mataifa FAO fedha ambazo zitatumiwa katika kushughulikia hali iliyopo.