Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwachilieni mwanamke wa kipalestina aliye katika mgomo wa kula:UM

Mwachilieni mwanamke wa kipalestina aliye katika mgomo wa kula:UM

Mwakilishi maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa hali ya haki za binadamu kwenye himaya ya Palestina inayokaliwa tangu 1967 Richard Falk, ameelezea hofu yake kuhusu Hana Shalabi mwanamke wa Kipalestina anayeshikiliwa na Israel ambaye kwa sasa yuko kwenye mgomo wa kula kwa karibu mwezi mzima.

Bwana Falk amesema hali ya Bi Shalabi ni mbaya na ya kutishia maisha ametoa ombi la kuzingatia utu na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kwa niaba yake, ili Isreal ifikirie kumaliza vitendo visivyo vya kibinadamu dhidi ya Bi Shalabi na kumwachilia mara moja.

Bwana Falk amesema mgomo wa kula kwa Bi Shalabi ni dhidi ya kushikiliwa bila mashitaka na Israel, kuteswa wakati alipokamatwa, njia iliyotumika kumhoji na mchakato mzima wa kumuweka kizuizini.

Bi Shalabi alikamatwa Februari 16 na amekuwa katika mgomo wa kula tangu wakati huo.

 Wazazi wa Bi Shalabi mama yake mwenye miaka 65 na baba yake miaka 67 nao wako katika mgomo wa kula tangu Februari 23.