Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Coomaraswamy akaribisha hukumu ya kwanza ya ICC dhidi ya kuingiza watoto jeshini

Coomaraswamy akaribisha hukumu ya kwanza ya ICC dhidi ya kuingiza watoto jeshini

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto kwenye migogoro ya silaha Bi Radhika Coomaraswamy amesema leo ukwepaji sheria umefikia tamati kwa mbabe wa kivita Thoams Lubanga na wote wanaoingiza na kutumia watoto jeshini.

Bi Coomaraswamy amepongeza hukumu hiyo ya kwanza kabisa ya mahakama ya ICC na kusema huu ni wakati wa mawasiliano ya kimataifa na wababe wote na makamanda duniani watapata taarifa ya hukumu ya Lubanga na kuwapa tahadhari.

Mamia ya watoto waliingizwa jeshini na kupatiwa mafunzo ya kuuwa, kubaka, na kutesa chini ya uongozi wa Thomas Lubanga kati ya mwaka 2002 na 2003.

Na kuwaingiza jeshini watoto wa chini ya umri wa miaka 15 ni uhalifu wa kivita chini ya mkataba wa Roma.

Bi Coomaraswamy ameongeza kuwa wakati utoto wa waliochukuliwa na Lubanga umepotea daima anatumaini kuwa haki iliyotendeka leo itawasaidia kufunga ukurasa na kuendelea na maisha yao.

Amemesema anatumai mahakama itatoa fidia kwa waathirika na jamii zao katika kutambua athari walizopata.