Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yalaani mashambulizi kwenye kambi ya Lou Nuer

UNMISS yalaani mashambulizi kwenye kambi ya Lou Nuer

 

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umepokea taarifa zinazoashiria kwamba mashambulizi yamefanyika na watu wasiojulikana dhidi ya makambi kadhaa ya Ng’ome Lou Nuer kwenye maeneo ya karibu na mpaka wa Sudan Kusini na Ethiopia.

UNMISS imetuma timu ya kushika doria na wauguzi kwenye maeneo ya Akobo na Wanding ili kutanabahi mazingira ya mashambulizi hayo na kutoa msaada wa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na uongozi wa eneo hilo makambi mengi ya ng’ombe yaliyoshambuliwa yapo ndani ya Ethiopia. Taarifa zinaonyesha kwamba majeruhi 63 wanatibiwa hospitali ya Akobo, lakini idadi kamili ya majeruhi ikiwemo waliouawa bado haijajulikana.

UNMISS imelaani vikali mashambulizi haya na kutoa wito kwa jamii zote za Jonglei kujizuia na kukomesha machafuko ya kijamii ambayo tayari yameshasababisha madhara makubwa ikiwemo kupotea kwa maisha ya watu.

Mashambulizi haya yamekuja wakati ambao serikali ya Sudan Kusini imeteua tume ya amani itakayojikita kurejesha amani na maridhiano baina ya jamii za Jonglei. Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini Hilde F. Johnson amezitaka jamii za Jonglei kushirikiana na kuhakikisha mipango muhimu ya amani inatekelezwa na kufanikiwa.