Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la mahitaji na mabadiliko ya hali ya hewa yanatishia raslimali ya maji

Ongezeko la mahitaji na mabadiliko ya hali ya hewa yanatishia raslimali ya maji

Ongezeko kubwa la mahitaji ya maji duniani linatishia malengo yote ya maendeleo, imeonya ripoti ya karibuni ya Umoja wa mataifa kuhusu maendeleo ya maji iitwayo “kudhibiti maji wakati wa hatari na shinikizo”.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa Jumatatu mjini Marseille Ufaransa na mkurigenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO Irina Bokova na mwenyekiti wa kitengo cha maji cha Umoja wa Mataifa UN-Water Michael Jarraud inasema ongezeko la mahitaji ya chakula, ukuaji wa haraka wa miji na mabadiliko ya hali ya hewa vinaongeza shinikizo katika usambazaji wa kimataifa wa maji.

Ripoti imeongeza kuwa hali hii tata inahitaji kutafakari upya njia za kuweza kuudhibiti rasilimali ya maji duniani na kusema maji salama hayatumiki ipasavyo kwa mujibu wa mahitaji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo watu katika maeneo mbalimbali ya dunia wanapata fursa ya maji safi ya kunywa hivi sasa huku asilimia 86 ya watu katika nchi zinazoendelea watakuwa na rasilimali hiyo ifikapo 2015, lakini imeonya kwamba bado maji taka kama hayakusanywi ipasavyo au kutiwa dawa na kusafishwa.