Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen inapaswa kuendelea na mageuzi katika hali ya amani na utulivu:UM

Yemen inapaswa kuendelea na mageuzi katika hali ya amani na utulivu:UM

Taifa la Yemen ambalo hivi karibuni lilifaulu kuendesha uchaguzi wa rais katika mazingira huru na ya amani, linapaswa kuendelea kushikilia mkondo huo huo wa mageuzi salama na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizosalia kwa mustakabala wa watu wake.

Yemen mapema mwezi uliopita, ilifanya uchaguzi ulioshuhudia mamia kwa maelfu ya wananchi wakimiminika kwenye vituo vya kupigia kura.

Katika uchaguzi huo Bwana Abbed Rabbo Mansour al-Hadi aliibuka mshindi.

Akitizama hali jumla ya mambo nchini humo, mjumbe maalum wa katibu mkuu nchini humo Jamal Benomar amesema kuwa wakati wa kurudi nyuma sasa umekwisha na kilichosalia sasa ni kuendelea na mageuzi ambayo yanakaribisha enzi mpya ya maridhiano.

Mjumbe huyo amewapongeza wananchi wa taifa hilo kwa kujitokeza kwa wingi kwenye upigaji kura na kusema kuwa hiyo ni ishara njema ya uanzishwaji wa harakati za ujenzi mpya wa taifa hilo.