Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNESCO alaani mashambulizi dhidi ya kituo cha habari Homs Syria:

Mkuu wa UNESCO alaani mashambulizi dhidi ya kituo cha habari Homs Syria:

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Irina Bokobva, Alhamisi amelaani vikali mashambulizi ya jeshi la Syria dhidi ya kituo cha habari mjini Homs. Shambulio lilifanyika tarehe 22 Februari na kusababisha vifo vya waandishi habari wawili na kujeruhi wengine wengi.

Bi Bokova ameutaka uongozi wa Syria kuheshimu hadhi ya waandishi wa habari na kulinda usalama wao. Waandishi waliouwawa katika shambulio hilo ni ripota wa Marekani wa habari za vita Marie Colvin na mpiga picha wa Ufaransa Remo Ochlik.

Mkuu huyo wa UNESCO amesema anahofia waandishi wengine waliojeruhiwa na kuitaka serikali ya Syria na majeshi yaliyo na silaha kuheshimu uhuru wa habari na waandishi katika maeneo ya vita. Amesema kushambulia waandishi kunapingana na mkataba wa Geneva ambao Syria imetia saini, pia azimio la baraza la usalama namba 1738 kuhusu kulinda waandishi habari katika maeneo ya vita.

Marie Colvin alikuwa akiishi uingereza na amekuwa akiripotia gazeti la uingereza la The Sunday Times. Vifo vya waandishi hao vimefanya idadi ya waandishi habari waliouawa tangu kuzuka machafuko Syria kufikia 6.