Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM aitaka Morocco kutekeleza sera zinazozingatia usawa wa kijinsia

Mtaalamu wa UM aitaka Morocco kutekeleza sera zinazozingatia usawa wa kijinsia

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu ameitolea mwito Morocco kuweka mipango mahususi kwa shabaha ya kusogeza mbele mafanikio ya wanawake hasa kwa kuyatupia macho maeneo ya kisheria ambayo yanakwamisha ustawi wao.

Kamala Chandrakirana amesema kuwa mifumo ya kisheria na taratibu zilizopo nchini Morocco siyo tu zinawaweka  wanawake kando, lakini pia zinaacha makundi mengine ya watu ikiwemo wafanyakazi wa majumbani na makundi ya wahamiaji katika mazingira hatarishi .

Makundi hayo yanatajwa kuwa hatarini kuvunjwa kwa haki zao za msingi ikiwemo zile zinazogusa maeneo ya kibinadamu, hivyo serikali hiyo ya Morocco imehimizwa kuchunguza upya mwenendo wake.

Pamoja na kuunga mkono hatua kadhaa zilizopigwa hasa kwenye maeneo ya kuanzisha mpango wa uandikwaji upya wa baadhi ya sheria, lakini hata hivyo mtaalamu huyo ametaka zingatio la pekee hasa wakati huu ambako miito ya kuwawezesha wanawake ikizidi kupazwa.