Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la UM juu ya ukuzaji sekta ya madini lafikia tamati Tanzania

Kongamano la UM juu ya ukuzaji sekta ya madini lafikia tamati Tanzania

Kamishna ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya uchumi kwa kanda ya afrika, imehitimisha mkutano wake wa 16 jijini Dar es salaam ambako imesisitiza haja ya kuimarisha sekta ya madini kwa ajili ya kukuza maendeleo barani humo.

(SAUTI GEORGE NJOGOPA)

Mkutano huo ulioduma kwa muda wa juma moja, umewaleta pamoja mawaziri wa masula ya madini, watunga sera, wawakilishi kutoka nchi za Ulaya, pamoja na makundi mengine ya kimaendeleo.

Nchi ambazo makampuni yake yametuwama barani Afrika yakijishughulisha na mikataba ya utafutaji madini, zimepata fursa kwenye mkutano huo kwa kutuma wajumbe kadhaa, ambao wote kwa pamoja wameshiriki majadiliano yaliyolenga kukuza sekta ya madini.

Waziri wa nishati na madini wa Tanzania Bwana William Ngeleja, amesema kuwa mada zilizojadiliwa kwenye kongamano hilo, zinatoa mwongozo mpya, mwongozo ambao unamulika moja kwa moja kwenye usimamizi sahihi wa rasilimali zilizopo barani Afrika.

Katika wakati huu ambako nchi za Afrika zikilaumiwa kwa kuingia kwenye mikataba mibovu na makampu ya ng’ambo, mkutano huo umekosoa mwenendo huo, lakini ukatoa mwongozo mpya ukitaka kwa kila nchi kuanzisha mufumo ya upitiaji wa mikataba hiyo.

Mkutano huo unafuatia ripoti ya wataalamu wa maendeleo waliowasilisha hivi karibuni, ripoti ambayo imemulika na kutoa mapendekezo yanayohimiza kuwepo kwa wataalamu wa kizalendo ambao watatoa mchango mkubwa kwenye uendelezwaji wa sekta hizo za madini na nishati.