Watu takribani 35,000 wasio na makazi nchini Hungary wanakabiliwa na faini na vifungo kufuatia hatua ya bunge la nchi hiyo kupitisha sheria zinazofanya hali ya kutokuwa na makazi kama ni uhalifu au kosa la jinai.
Wataalamu wawili wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wanasema sheria hizo zinazopinga hali ya kutokuwa na makazi sio tuu kwamba ni za kibaguzi bali pia zinaweza kuwa zinakiuka haki za msingi za wale wanaoishi katika umasikini.
Magdalena Sepulveda mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu umasikini uliokithiri na haki za binadamu anasema matatizo ya kifedha na kiuchumi yamechangia wimbi la watu wasio na makazi nchini Hungary ambao wanahitaji kusaidiwa na sio kuchukuliwa kama wahalifu. Naye mtaalamu kuhusu haki ya kuwa na makazi bora Raquel Rolnik amesema kuwatia mbaroni wasio na makazi sio suluhisho, akiongeza kwamba serikali zinawajibu wa kuhakikisha zinatoa makazi kwa watu wake wanohitaji msaada.
Wataalamu hao wamesema ukizingatia gharama kubwa za polisi, mahabusu, kuendesha kesi na kufunga watu, fedha hizo zingetumika vizuri kupata suluhisho la wasio na nyumba katika jamii.