Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Kaskazini mwa Kosovo imetulia lakini bado ni ya hatihati

Hali Kaskazini mwa Kosovo imetulia lakini bado ni ya hatihati

Juhudi za kutuliza mvutano Kaskazini mwa Kosovo zimezaa matunda lakini hali bado haijatengamana kabisa. Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Edmond Mulet alipotoa taarifa kwenye Baraza la Usalama leo Jumatano. Kosovo jimbo la zamani la Serbia ilijitangazia uhuru mwaka 2008 na kuwa taifa lililojitenga, lakini sehemu ya Kaskazini mwa nchi hiyo wakazi wake wengi ni kabila la Waserbia ambao walikana kujitenga, na hili limesababisha kuendelea kwa mapigano baiana ya wakazi wa Kiserbia na majeshi ya NATO nchini humo.

Mulet amesema hata hivyo kwa ujumla hali imeimarika na majadiliano yanayoongozwa na muungano wa Ulaya mjini Brussels kati ya Kosovo na Serbia yameanza. Kosovo na Serbia wamekuwa na mvutano unaoendelea kuhusu udhibiti wa maeneo mawili ya mpaka Kaskazini mwa Kosovo mvutano ambao umesababisha machafuko kati ya wakaazi Waserbia na vikosi vya NATO.