Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watu kukabiliwa na njaa Sudan Kusini

Mamilioni ya watu kukabiliwa na njaa Sudan Kusini

Mamilioni ya watu Sudan Kusini watakabiliwa na njaa mwaka huu endapo hatua za haraka hazitochukuliwa, imesema ripoti ya pamoja iliyotolewa na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa.

Shirika la chakula na kilimo FAO na shirika la mpango wa chakula duniani WFP yameonya kwamba hali ya usalama wa chakula Sudan Kusini inajongea haraka katika kiwango cha matatizo ambayo dunia haiwezi kumudu kuipuzia. Ripoti inasema zaidi ya watu milioni 4.7 wanakabiliwa na upungufu wa chakula mwaka huu ikiwa imeongezeka kutoka milioni 3.3 ya mwaka 2011.

Mvua hafifu, vita na watu kutawanywa na machafuko kumechangia mavuno haba, hata hivyo idadi kubwa ya watu wanaorejea nyumbani Sudan Kusini baada ya kupatikana uhuru imeongeza mahitaji ya chakula na kusababisha bei kupanda kiasi cha wengi kutomudu kununua. WFP na FAO wanaonya kwamba idadi ya watakaohitaji msaada wa chakula itaongezeka mara mbili katika miezi michache ijayo na yanatafuta kuchangisha fedha kiasi cha dola milioni 183 ili kutoa msaada wa dhara na kusaidia upande wa kilimo kwa jamii zilizoathirika.