Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanamuziki wa Uingereza Sarah Brightman awa msanii wa amani wa UNESCO

Mwanamuziki wa Uingereza Sarah Brightman awa msanii wa amani wa UNESCO

 Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limetangaza leo kwamba mwanamziki na muigizaji huo wa Uingereza atajiunga kwenye orodha ya wasanii wengine wa amani ambao wanatumia umaarufu wao na mchango wao wa kisanii kuchagiza programu na ujumbe wa UNESCO.

Bi Brightman atatawazwa rasmi kuwa msanii wa amani katika hafla maalum itakayofanyika makao makuu ya UNESCO Paris Jumatano.

UNESCO imechangua mwanamziki huyo kutokana na mchango wake mkubwa katika masuala ya kibinadamu na kazi za kujitolea katika miaka yote ya usanii wake, jinsi anavyochagiza maingiliano ya tamaduni na kubadilishana uzoef wa tamaduni zingine, pia jinsi anavyotoa muda wake kwa mawazo na malengo ya UNESCO.

Bi Brightman anajulikana kwa kuwa na sauti nzuri ya kuimba tangu alipoanza usanii huo miaka ya 1980. Amepata mafanikio makubwa katika fani ikiwa ni pamoja na kuuza zaidi ya CD na DVD milioni 30 duniani kote.

Wasanii wengine wa UNESCO kwa ajili ya amani ni Celine Dion mwanamziki kutoka Canada, Msanifu majengo kutoka Iraq Zaha Hadid, Mwanamuziki wa Brazil Gilberto Giland na mnenguaji kutoka Uhispania Joaquin Cortes.