Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii 2000 zaidi za Kiafrika zatokomeza ukeketaji mwaka 2011:UNFPA

Jamii 2000 zaidi za Kiafrika zatokomeza ukeketaji mwaka 2011:UNFPA

Takribani jamii 2000 barani Afrika zimeachana na mfumo wa ukeketaji kwa wanawake mwaka 2011. Hatua hii imefanya idadi ya jamii zilizotokomeza mila hiyo barani Afrika kufikia 8000 katika miaka michache iliyopita.

Takwimu hizi zimetokana na utafitio uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA na shirika la moja wa Mataifa la khudumia watoto UNICEF. Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa UNFPA Bababatunde Osotimehin aliyezungumza katika siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji inayoadhimishwa Februari 6 kila mwaka, matokeo ya utafiti huo yanatia moyo na kudhihirisha kwamba mila na utamaduni potovu unaanza kubadilika na jamii zinaungana kulinda haki za wasichana na wanawake.

Ametoa wito kwa jamii zote kujiunga na juhudi za kutokomeza ukatili huo na kusaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya wanawake na wasichana duniani. Kila mwaka takribani wasichana na wanawake milioni 3, au wasichana 8000 kila siku wako katika hatari ya kukeketwa, na inakadiriwa kwamba wasichana na wanawake milioni 130 hadi milioni 140 wamekeketwa hususani barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.