Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi na Uchina wapinga azimio la UM kuhusu Syria

Urusi na Uchina wapinga azimio la UM kuhusu Syria

Urusi na Uchina wamepiga kura leo kupinga azimio kuhusu Syria kwenye Baraza la Usalama, huku wajumbe wengine 13 wamepiga kura ya kuliunga mkono azimio hilo. Azimio hilo limelaani kuendelea kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaotekelezwa na serikali ya Syria.

Pia limezitaka pande zote nchini humo yakiwemo makundi ya watu wenye silaha kusitisha ghasia au wawajibishwe. Kura mbili za turufu zilizopigwa na Urusi na Uchina zimewakasirisha baadhi ya nchi wanachama akiwemo balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Susan Rice.

(SAUTI YA SUSAN RICE)

“Kwa miezi kadhaa sasa baraza hili limewekwa mateka na baadhi ya nchi wanachama. Wanachama hawa wanatoa madai yasiyo ya msingi na wanapigania masilahi binafsi huku wakichelewesha na kupinga maandiko yoyote ambayo yatamshinikiza Assad kubadili vitendo vyake. Hatua hii ni aibu kubwa hasa ukifikiria kwamba mmoja wa wajumbe hawa anaendelea kupeleka silaha kwa Assad.”

Rice amesema raia 3000 zaidi wameuawa tangu Urusi na Uchina walipopiga kura ya turufu dhidi ya azimio la Syria mwezi Oktoba mwaka jana.