Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaeleza wasi wasi wake kufuatia ripoti za kuteswa kwa wakimbizi nchini DRC

UNHCR yaeleza wasi wasi wake kufuatia ripoti za kuteswa kwa wakimbizi nchini DRC

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeelezea wasi wasi wake kufuatia ripoti za hivi majuzi kuwa wakimbizi wa ndani wameteswa na kuuawa na makundi yaliyojihami kwenye kambi za wakimbizi wa ndani kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Tangu mwanzo wa mwaka 2011 makundi yaliyojihami yamekuwa yakivamia kambi za wakimbizi wa ndani kwenye mkoa huo zikiwemo za Nyanzale, Mweso na Birambizo. Wakimbizi kwenye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kila mara wako kwenye hatari ya kushambuliwa na makundi kadha yaliyojihami yanayowalaumu kwa kushirikiana na kundi moja au lingine.