UM wawataka raia wa DR Congo kuepuka ghasia kwa kutatua mzozo wa kura kwa njia ya amani

2 Februari 2012

Wakati matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa bunge nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yametangazwa Umoja wa Mataifa leo umewachagiza wahusika wote kutumia njia za kisheria kutatua madai yote ya uchaguzi na kujizuia kutumia nguvu au ghasia.

Mamilioni ya raia wa Congo walipiga kura tarehe 28 Novemba mwaka jana kuchagua Rais na wabnge. Wakati matangazo ya Urais yalitangazwa awali, tume huru ya uchaguzi ya nchi hiyo CENI imetangaza matokeo ya uchaguzi wa bunge wa majimbo 162 kati ya majimbo 169 Januari 26 na Februari mosi mwaka huu.

Na kwa mujibu wa mpango wa kulinda amani nchini humo MONUSCO tume ya uchaguzi imefuta matokeo ya majimbo saba yaliyosalia.

MONUSCO imekaribisha hali ya utulivu na amani ambayo imejitokeza nchi nzima tangu kutangazwa kwa matokeo hayo. Pia mpango huo umezikumbusha pande zote husika kwamba unaendelea kufuatilia kwa karibu ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya ghasia vinavyotekelezwa kwa misingi ya uchaguzi huo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud