Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA awasili Juba Sudan Kusini

Mkuu wa OCHA awasili Juba Sudan Kusini

Katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu Sudan Kusini mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Valarie Amos amekutana na wawakilishi wa mashirika ya misaada mjini Juba.

Bi Amos na wawakilishi hao wamejadili changamoto mbalimbali za kibinadamu zinazolikabili taifa hilo changa ikiwa inajongea miezi sita tangu ijipatie uhuru wake.

Katika ziara hiyo pia atatathimini hali ya kibinadamu nchi humo na kuitanabaisha jumuiya ya kimataifa changamoto zilizopo.

Sudan Kusini inakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo maelfu ya watu waliotawanywa mwaka 2011, mamia ya watu wanaorejea kutoka Sudan na wimbi la wakimbizi waliosababishwa na machafuko yanayoendelea kwenye jimbo la Kordofan Kusini na Blue Nile.

Licha ya hayo mapigano, umasikini na matatizo ya chakula yanaleta athari kubwa katika maisha ya watu nchini humo. Mashirika ya misaada yamemweleza bi Amos juhudi za ugawaji wa misaada ya kibinadamu kwenye jimbo la Jonglei lililokumbwa na machafuko hivi karibuni.

Tarehe 2 Amos atazuru Jonglei ambako atashuhudia operesheni za misaada na kukutana na wawakilishi wa serikali na mashirika ya misaada kabla ya tarehe 3 kukutana na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, waziri wa masuala ya kibinadamu na majanga Joseph Lual Acuil.