Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wa Baraza la Usalama watofautiana kwa utekelezaji wa mswaada wa azimio kuhusu Syria

Wajumbe wa Baraza la Usalama watofautiana kwa utekelezaji wa mswaada wa azimio kuhusu Syria

Maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani, Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa waliokutana Jumanne jioni katika kikao maalumu cha Baraza la Usalama kutoa shinikizo la kupitisha mswaada wa azimio litakalounga mkono mipango ya Umoja wa nchi za Kiarabu kuhusu suala la Syria watofautiana. Mswada huo wa azimio unamtaka Rais Al-Assad kujiuzulu kama sehemu ya kipindi cha mpito cha kidemokrasia.

Wakati huohuo wajumbe wengine wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama Urusi na Uchina wameendelea kupinga hatua yoyote inayotaka kuleta mabadiliko ya uongozi Syria, hatua za kutumia nguvu au mataifa ya nje kuingia siasa za ndani za Syria. Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Churkin ameonya kwamba uingiliaji wa aina kama hiyo utachochea vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuleta adha katika eneo zima. Pia amesema Urusi itatumia kura ya turufu endapo kura yoyote ya azimio dhidi ya Syria itapigwa. Nayo Togo ambayo inashikilia Urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu kuanzia Februari Mosi imesema itajikita katika kuhakikisha amani nchi Syria na Afrika. Balozi wa Togo kwenye Umoja wa Mataifa Kodjo Menan amesema taifa lake litakuwa na jukumu muhimu.

(SAUTI YA KODJO MENAN)