Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakenya wanne kujibu mashitaka ya ICC ya ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya

Wakenya wanne kujibu mashitaka ya ICC ya ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya

 Wanasiasa wanne wa Kenya kujibu mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC iliyoko The Hage Uholanzi. Mahakama ya ICC imewakuta na kesi ya kujibu Wakenya hao ambao ni naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta, aliyekuwa waziri William Ruto, mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura na mwandishi wa habari Joshua Sang.

Majaji wa mahakama hiyo wamesema kuna mazingira ya kuamini kwamba mauaji, ubakaji na makosa mengine ya kuwatimua watu kwa nguvu vilitekelezwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Hata hivyo ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka dhidi ya aliyekuwa waziri Henry Kosgei na mkuu wa zamani wa polisi meja jenerali mustaafu Mohammed Hussein Ali hautoshelezi kuwafungulia mashitaka wawili hao. Akitoa uamuzi wa kesi ya kujibu dhidi ya wanne hao kwa niaba ya jopo la majaji, jaji Ekaterina Trendafilova amesema

(SAUTI YA EKATERINA TRENDAFLOVA)

Watu zaidi ya 1500 waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007 na wengine  maelfu kulazimika kuzikimbia nyumba zao. Mmoja wa majaji Hans-Peter Kaul amekataa kuunga mkono kesi ya waendesha mashitaka akisema ingawa makosa ni makubwa chini ya sheria za Kenya, hayakuwa uhalifu dhidi ya binadamu kama yanavyoelezwa kwenye mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama ya ICC.