Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yataka kuongezwa shabaha ya kufikia maendeleo endelevu

UM yataka kuongezwa shabaha ya kufikia maendeleo endelevu

Wakati ambapo mwaka kwa ajili ya kutoa zingatio la maendeleo endelevu ukianzishwa rasmi, Umoja wa Mataifa umetaka mataifa pamoja na taasisi za kibinasfi kuweka shabaya ya pamoja ili kusukuma mbele juhudi zinazopalilia upatikanaji wa suluhu ya pamoja juu ya matumizi ya nishati endelevu.

Takwimu za hivi punde zinaonyesha kuwa katika uso wa dunia, kila mtu mmoja kati watu saba, bado anakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nishati ya kisasa ya umeme na hali inavyoonekana huenda ikapindukia katika siku za usoni.

Kwa mantiki hiyo Umoja wa Mataifa unazitaka serikali, mashirika ya kiraia pamoja na sekta binafsi kuongeza juhudi na mashirikiano ya karibu ili kufanikisha mapinduzi ya nishati mbadala ambayo itatoa ustawi mwema kwa dunia.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kimataifa unaojadilia juu ya suala la nishati endelevu huko Abu Dhabi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuwa kuwepo kwa ujumbe wa kimataifa kwenye mkutano huo kunadhihirisha umuhimu wa suala hilo.