Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waandaa mikakati kuimarisha serikali Somalia

UM waandaa mikakati kuimarisha serikali Somalia

Mkurugenzi wa masuala ya kisiasa katika Umoja wa Mataifa B. Lynn Pascoe leo ameliambia Baraza la usalama kwamba jamii ya kimataifa ihakikishe nchi hiyo inapata katiba mpya mwezi wa Mei, halafu ifanye uchaguzi wa bunge, spika na raisi, kama ilivyopendekezwa katika mkataba uliyosainiwa mjini Kampala na waakilishi wa taasisi za serikali na makundi mbali mbali ya Kisomali mwaka uliopita.

Hatua hizo zitafuatiwa na juhudi za kuhakikisha udhibiti wa serikali katika maeneo yaliyoko kaskazini mwa nchi yanayomilikiwa na kundi la Al-Shabaab kwa sasa, amesema Bw. Pascoe katika maelezo yake kwa Baraza la usalama kuhusu hali nchini Somalia.

Baraza limependekeza pia juhudi zifanyike kuboresha utawala kwa kuhakikisha kuna utumishi wa umma imara.

Bwana Pascoe amesema mpango wa kuthibiti usalama pia umekamilishwa na unasubiri idhini ya bunge la mpito lililoko sasa, huku mbinu zikiandaliwa kupanua nafasi za biashara.

Ameisihi jamii ya kimataifa kuzidisha misaada yake kwa Somalia ili kuakikisha mipango hiyo ya kumaliza hali ya vurugu na mapigano nchini Somalia inatekelezwa kama iliyopangwa na Umoja wa Mataifa na washirika wake, wakiwemo Muungano wa Afrika, IGAD na nchi wafadhili.

Masuala hayo yote yatajadiliwa kwa kina katika mkutano wa kimataifa utakaofanywa mjini London mwezi ujao, amesema Bwana Pascoe.

Katika taarifa yake kwa Baraza la usalama, Kamishina wa Amani na Usalama wa Muungano wa Afrika, Ramtane Lamamra, amesema uamuzi wa Kenya kutoa majeshi yake kujiunga na jeshi la Muungano wa Afrika la kulinda usalama Somalia, AMISOM, pamoja na harakati za Ethiopia dhidi ya Al-Shabaab zimesaidia kukombolewa maeneo mapya.

Ametoa wito kwa Wasomali walinde maeneo hayo, huku wakizidisha juhudi za amani baina yao.