Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan inaweka vikwazo kwa walinda amani Darfur

Sudan inaweka vikwazo kwa walinda amani Darfur

Vikwazo vinavyowekwa na serikali ya Sudan vimeathiri pakubwa shughuli za mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika Darfur UNAMID.

Mkuu wa masuala ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa Herve Ladsous ameliambia Baraza la Usalama Jumatano kwamba kumekuwa na ongezeko la mapigano baina ya serikali na wajeshi ya waasi katika wiki za karibuni.

UNAMID ilianzishwa mwaka 2007 kuwalinda maelfu ya raia waliotawanywa na machafuko Darfur. Bwana Ladsous amesema serikali ya Sudan imekuwa ikiwazuia wafanyakazi wa UNAMID kwenda katika baadhi ya maeneo. Amesema vikwazo hivyo ni pamoja na vya ndege, na kushika doria katika maeneo yenye mapigano kuanzia Desemba hadi mwanzo mwa mwaka huu na vikwazo vimewekwa kwa kuzingatia operesheni za jeshi la Sudan. Vikwazo hivyo vimeathiri sana uwezo wa UNAMID kutimiza majukumu yake na kupeleka timu katika maeneo yaliyoathirika.

Maelfu ya watu wameuuawa katika machafuko ya Darfur ambayo pia yamewafungisha virago watu takribani milioni 2 tangu kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe Darfur mwaka 2003.