Ban akaribisha hatua ya uondoaji wa hali ya hatari nchini Fiji

5 Januari 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha kwa furaha uamuzi wa serikali ya Fiji iliyotangaza kuondoa hali ya hatari iliyoiweka mwaka 2009, akisema kuwa kitendo hicho kinatoa mkono wa matumaini unaorejesha mfumo wa kikatiba katika eneo hilo lililopo kusin mwa Pacific.

Duru kutoka ndani ya serikali ya Fiji zinasema kuwa hali hiyo ya hatari inatazamiwa kuondolewa rasmi mwishoni mwa juma.

Katika taarifa yake iliyotolewa kupitia msemaji wake, Ban amepongeza uamuzi huo aliouita ni wa kutia matumaini kuhusu urejeshwaji wa mfumo unaozingatia matakwa ya katiba lakini pia ametaka kuwepo kwa ushirika wa dhati toka kwa makundi yote wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa mpito.

Amesisitiza kuwa ni lazima kuwepo kwa meza ya majadiliano tena itayochukua utashi wa makundi yote ili kufanikisha uchaguzi ulio usoni.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud