Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu hatua ya kuwepo kwa mazungumzo kwa Israel na Palestina

Ban asifu hatua ya kuwepo kwa mazungumzo kwa Israel na Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesifu juu ya kuwepo kwa mazungumzo ya kuendelea kusaka amani baina ya Palestina na Israel, mazungumzo yaliyofanyika huko Amman, Jordan yakihudhuriwa pia na wanadiplomasia kadhaa.

Ban hata hivyo amezitolea mwito pande zote mbili kuwa mkutano huo unapaswa kuchukuliwa kama fursa ambayo itafungua mlango wa kufanyika majadiliano zaidi katika siku za usoni.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa mashariki ya kati Robert Serry akiwa na wawakilishi wa pande hizo mbili, pamoja na ujumbe wa pande nne unaoangazia hali ya eneo hilo Quarte, wamekuwa na mkutano wa pamoja ambao umeangazia hatua jumla za kusaka amani.

Pamoja na kuzipongeza pande hizo mbili,Ban pia amemtumia salamu za pongezi mfalme wa Jordan kwa kufaulu kuzileta pamoja pande hizo na kuwa na majadiliano ya ana kwa ana.

Majadiliano ya ana kwa ana kwa pande zote mbili yalivunjika Septemba 2010 kufuatia hatua za Israel kuendelea na makazi ya walozi wake kwenye ardhi ya Palestina.