Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabalozi wa Umoja wa Ulaya waitaka Israel kusitisha mpango wa ujenzi wa makazi ya walowezi

Mabalozi wa Umoja wa Ulaya waitaka Israel kusitisha mpango wa ujenzi wa makazi ya walowezi

Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya ambao wanaziwakilisha nchi zao kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameitaka Israel kusitisha mara moja mpango wake wa ujenzi wa makazi ya walowezi katika mipaka ya Palestina ikiwemo pia eneo la Jerusalemu Mashariki.

Katika taarifa yao ya pamoja, mabalozi hao wamesema kuwa kuendelea na ujenzi wa makazi ya kudumu kwenye eneo hilo ni jaribio linalohatarisha nafasi ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo baina ya pande zote mbili Palestina na Israel.

Mabalozi hao kutoka nchi za Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Ureno wameelezea kusikitishwa kwao na namna Israel inavyokaidi miito ya usitishwaji wa ujenzi wa makazi ya raia wake katika ardhi inayokalia kwa nguvu ya Palestina.

Mazungumzo ya kusaka suluhu ya kudumu yalivunjika kufuatia hatua ya Israel kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa makazi mapya kwa raia wake.