UM na washirika wake wataka viongozi Somalia kumaliza mvutano dhidi ya spika wa bunge

19 Disemba 2011

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika na mashirika ya kikanda wamezitaka taasisi za serikali ya mpito ya Somalia kutatua haraka mvutano wa kisiasa kufuatia kura ya bunge ya wiki iliyopita ya kutokuwa na imani na spika Sharif Hassan Sheikh Aden.

Taarifa iliyotolewa na ujumbe huo wa pamoja inasema tunawataka viongozi wa taasisi za serikali ya mpito, wabunge na wadau wote kuepuka matamko au hatua zozote zitakazochochea zaidi hali ya mvutano ambayo ipo na kuongeza zahma.

Ujumbe huo ambao ulikwenda Somalia kukutana na uongozi wa serikali Jumamosi umejumuisha naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha Rose-Migiro, Christian Manahl naibu mwakilishi wa Katibu Mkuu Somalia, Boubacar Diarra mwakilishi maalum wa mwenyekiti wa muungano wa Afrika na Kipruto Arap Kirwa mapatanishi wa Somalia wa uongozi wa maendeleo wa kikanda IGAD.

Ujumbe umeelezea hofu ya jumuiya ya kimataifa kuhusu mgogoro wa kisiasa kwa viongozi wa serikali ya mpito ukisisitiza kwamba mkwamo wowote utakuwa na athari kubwa katika kurejesha amani na utulivu kwa taifa hilo ambalo halina serikali ya kudumu tangu mwaka 1991.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter