Pillay alaani matumizi ya nguvu kwa waandamanaji Misri

19 Disemba 2011

Kamishna wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay amelaani vikali hatua ya vikosi vya kijeshi kuyaandama na kuyasambaratisha maandamano ya amani yaliyowakusanyisha mamia ya wananchi walipanga kuelekea kwenye uwanja wa Tahrir mjini Cairo kupinga mwenendo wa utawala wa kijeshi.

Duru za habari zinasema kuwa zaidi ya watu 11 wamepoteza maisha na wengine 500 wakijeruhiwa tangu vikosi vya kijeshi vilipoanza kuyandama maandamano hayo ijumaa iliyopita.

Akielezea masikiti yake pamoja na shutuma zake kwa uongozi wa kijeshi wa Misri, Bi Pillay amesema kuwa kuwakuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuongeza kuwa vikosi vya kijeshi vimechukua hatua zilizodurufu ada ikiwemo kuwapinga na kuwabinya waandamanaji hao kitendo ambacho amesisitiza kuwa kinadhihirisha utawala wa kidhalimu.

Kadhalika ametoa mwito akitaka kuachiliwa mara moja kwa wale wanaoshikiliwa kutokana na kushiriki maandamano ya amani.

Tangu kuondolewa kwa utawala wa Hosn Mubarak baraza la kijeshi ndilo linaloendelea kushikilia madaraka ambalo hata hivyo hivi sasa linakabiliwa na lawama kali toka kwa makundi ya kiraia wakilitaka likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter