Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi wa UNESCO yuko Washington kuichagiza Marekani kurejesha msaada

Mkurugenzi wa UNESCO yuko Washington kuichagiza Marekani kurejesha msaada

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Bi Irina Bokova ameitaka Marekani kurejesha msaada wake kwa shirika hilo katika mkutano wake wa kwanza kati ya mingi anayotarajia kukutana na wabunge mjini Washington.

Katika majadiliano yake na wabunge Steny Hoyer na Gary Ackerman Bi Bokova ameelezea umuhimu wa kazi zinazofanywa na UNESCO duniani kulinda uhuru wa kujieleza, kuchagiza usalama wa waandishi wa habari, kuinua kiwango cha elimu ya wasichana na kuboresha mafunzo kwa waalimu miongoni mwa miradi mingi wanayoendesha.

Pia ametoa msisitizo katika kazi ya kupigia upatu masuala ya demokrasia na kuleta utulivu katika nchi ambazo Marekani ina maslahi. Amesema Marekani kukata msaada kunadhoofisha uwezo wa UNESCO kutekeleza mipango yake Iraq na Afghanistan maeneo ambayo ni muhimu sana kwa maslahi ya Marekani.