Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waitataka DRC kuyachukulia kwa uzito wa pekee malakamiko wakati wa uchaguzi mkuu

UM waitataka DRC kuyachukulia kwa uzito wa pekee malakamiko wakati wa uchaguzi mkuu

Umoja wa Mataifa umeitaka tume ya taifa ya Congo kuyachukulia katika uzito wa pekee malalamiko yaliyotolewa kuhusiana na uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni ambao ulilalamikiwa na baadhi ya waangalizi walioukosoa wakidai kuwepo kwa ukiukwaji wa kanuni.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na tume ya kikosi cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO, tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo inapaswa kuchukulia kwa uzito wa pekee hoja zilizotolewa kuhusiana na uchaguzi huo hasa kipengele kilicholalamikiwa mno kinachohusina na hatua za uhesabuji kura.

Katika taarifa yake, MONUSCO imesisitiza kuwa madai hayo lazima yatafutiwe ufumbuzi wa haraka tena kwa umakini mkubwa ili kujenga sura ya maridhiano na kuaminiana ndani ya wanchi wa Congo na hata katika maeneo mengine.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo wa wabunge na rais waangalizi mbalimbali ikiwemo wale wa kimataifa wametoa matamko wakikosoa mwenendo wa uchaguzi huo kwa kusema kuwa ulitawaliwa na kasoro kadhaa.