Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na watu wasio na utaifa wanastahili, kulindwa

Wakimbizi na watu wasio na utaifa wanastahili, kulindwa

Kamishina mkuu wa wakimbizi Antonio Guterres ametoa wito Jumatano wa kuwalinda wakimbizi na watu wasio na utaifa. Pia amesisitiza umuhimu wa kuwarusu watu wanaokadiriwa kuwa milioni 12 wasio na utaifa duniani kupata uraia na kufurahia haki za kuwa na utaifa.

Kamishina Guterres ameyasema hayo katika ufunguzi wa maadhimisho ya 60 ya mkataba wa wakimbizi na pia ni maadhimisho ya 50 ya mkataba wa kupunguza hali ya kutokuwa na utaifa. Amesema idadi ya watu waliolazimika kutawanyika kwa sababu moja au nyingine kufikia mwisho wa mwaka jana ni milioni 43.5 ikiwa ni ya juu kwa mwaka wa 15 mfululizo. Maelfu ya watu wametafuta hifadhi nje ya mipaka yao mwaka huu na idadi hiyo huenda ikaongezeka.

Guterres amesisitiza kwamba ulinzi kwa watu wanaouhitaji lazima uwepo na hasa ameonya juu ya matatizo ya kisiasa, hali ya uchumi, ubaguzi na chuki dhidi ya wageni.

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)